VOLUME 4, ISSUE 1

Title: Uchanganuzi wa Ruwaza za Toni katika Vitenzi Visoukomo Sahili vya Kirombo


Authors: Peter T Mramba

 Marco Edward Chuo Kikuu cha Mt. Augustino, Ndaki Shiriki Jordan Morogoro, Tanzania
*Correspondence: mrambadoctor@gmail.com


Abstract


Makala haya yanahusu uchanganuzi wa ruwaza za Toni katika Vitenzi visoukomo sahili vya Kirombo. Lengo kuu la makala haya ni kuchunguza ruwaza ya ujitokezaji wa toni katika vitenzi visoukomo sahili vya Kirombo na kanuni zinazotawala utokeaji huo. Aidha, malengo mahususi: kubainisha silabi inayohusishwa na Tonijuu Msingi (kuanzia sasa TJM) na mbili, kujadili ruwaza ya utokeaji wa toni katika vitenzi visoukomo sahili vya Kirombo na kanuni zinazotawala hutokeaji huo. Data ya Makala haya imetokana na utafiti mpana uliofanywa juu ya toni katika lugha ya Kirombo wilayani Rombo (2023) ambao uliongozwa na Nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru kwa kutumia Mkabala wa Tonijuu Msingi kama ulivyoasisiwa na Goldsmith (1976) na kuboreshwa na wanazuoni mbalimbali katika taaluma ya tonolojia. Aidha, mbinu za ukusanyaji data zilizotumika ni pamoja na mahojiano na ushuhudiaji. Katika mahojiano vitenzi visoukomo sahili viliandaliwa kwa Kiswahili na watoataarifa walihitajika kuvitamka kwa Kirombo huku mtafiti akirekodi na kualamisha toni katika vitenzi hivyo. Aidha, katika mbinu ya ushuhudiaji Mtafiti alishuhudia kwa kushiriki. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, kuna ruwaza mbalimbali za kitoni zinazoleteleza utokeaji wa kanuni za kitoni ambazo hutofautiana kutegemeana na idadi ya silabi. Ruwaza ya ujitokezaji wa toni katika vitenzi visoukomo sahili vya silabi mbili hadi sita, TJM hupachikwa katika silabi ya pili ya shina kutoka mwanzoni mwa neno. Aidha, kanuni anuwai kama vile usambaaji wa TJM kuelekea kulia mwa shina la kitenzi, uhamaji wa TJM, uradidi wa TJM na Udondoshaji wa kitamkwa, zimetekelezwa baada ya utekelezwaji wa kanuni ya jumla ya Upachikaji wa TJM, katika uibuzi wa ruwaza ya ujitokezaji wa toni katika umbo la nje kutoka umbo la ndani. Aidha, ruwaza ya ujitokezaji wa toni katika vitenzi vya idadi ya silabi mbili hadi sita vyote huanza na toni C katika KA ikifuatiwa ama na toni J au toni C katika silabi ya kwanza ya shina. Toni J hiyo usambaa hadi silabi ya mwisho kasoro mbili au moja kutoka mwishoni mwa shina la vitenzi husika.

Keywords: Arudhi ni sifa inayohusu mabadiliko ya vipambasauti kama vile kidatu, nguvumsikiko, tempo na lahani

Download the Article